Iran Yajibu Kauli ya Trump Kuhusu Umeme: “Dakika 30 Tu Nchi Itakuwa Na Giza Na Sio Kwa Miaka 25"

Afisa mkuu wa usalama wa Iran, Ali Larijani, amejibu kauli iliyotolewa na aliyekuwa rais wa Marekani Donald Trump kuhusu uwezo wa Marekani kuharibu miundombinu ya umeme ya Iran.

Larijani amesema kuwa ikiwa mashambulizi kama hayo yatatekelezwa, athari zake kwa Iran hazitakuwa kubwa kama inavyodaiwa na Trump.

Katika ujumbe aliouandika kwenye mtandao wa kijamii wa X, Larijani alieleza kuwa shambulizi lolote dhidi ya mfumo wa umeme wa Iran lingeweza kusababisha giza kwa muda mfupi tu, akitaja takribani dakika 30 kabla ya huduma kurejea tena.

Kauli hiyo imekuja baada ya Trump kusema katika hotuba yake kuwa Marekani ina uwezo wa kuharibu kabisa miundombinu ya umeme ya Iran ndani ya saa moja, hatua ambayo ingeifanya nchi hiyo ichukue hadi miaka 25 kujenga mfumo mpya wa uzalishaji na usambazaji wa nishati.

“Tunayo uwezo wa kutenganisha kabisa mfumo wao wa umeme ndani ya muda mfupi sana, na kuwafanya wachukue muda mrefu kuujenga upya,” Trump alinukuliwa akisema wakati akizungumza kuhusu nguvu za kijeshi na kiteknolojia za Marekani.

Hata hivyo, Larijani alipinga madai hayo kwa kusema kuwa hata kama tukio hilo lingetokea, hali ya giza nchini Iran ingedumu kwa muda mfupi sana. 

Alisema wataalamu wa Iran wana uwezo wa kurejesha mfumo wa umeme haraka kutokana na uwekezaji mkubwa uliowekwa katika teknolojia ya nishati na mifumo ya dharura.

Larijani pia alionya kuwa kukatika kwa umeme kunaweza kuwa na athari nyingine ambazo hazikutarajiwa na Marekani. 

Kwa mujibu wake, kuzimika kwa umeme katika maeneo ya kijeshi au vituo vya Marekani katika ukanda huo kunaweza kuathiri operesheni zao za usalama.

Alisema hali hiyo ingeweza kutoa “fursa kubwa” kwa vikundi au majeshi yanayopinga uwepo wa Marekani katika Mashariki ya Kati kuchukua hatua dhidi ya wanajeshi wa Marekani wanaoendesha operesheni katika eneo hilo.

Mvutano kati ya Iran na United States umeendelea kuongezeka katika miaka ya hivi karibuni, hasa kutokana na tofauti za kisiasa, kijeshi na kiusalama katika ukanda wa Mashariki ya Kati. 

Kauli za viongozi kutoka pande zote mbili zimekuwa zikiongeza mjadala kuhusu uwezekano wa mgogoro mkubwa zaidi.

Wachambuzi wa siasa za kimataifa wanasema vita vya kisasa havihusishi tu mashambulizi ya kijeshi ya moja kwa moja, bali pia vita vya kiteknolojia kama vile mashambulizi ya mtandao, uharibifu wa miundombinu muhimu na vita vya taarifa.

Kwa sasa, kauli hizi zimeendelea kuzua mjadala mkubwa duniani huku mataifa mengi yakifuatilia kwa karibu maendeleo ya mvutano huo na athari zake kwa usalama wa kimataifa.

Post a Comment

Previous Post Next Post