Iran Yatoa Tamko Zito Baada ya Marekani Kudaiwa Kukubali Masharti ya Amani

TEHRAN, Iran — Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran (SNSC) limetangaza kuwa taifa hilo limepata ushindi mkubwa dhidi ya maadui wake baada ya kudai kuwa Marekani imekubali masharti yaliyowekwa na Iran ya kusitisha vita kati ya pande hizo mbili.

Kupitia taarifa rasmi iliyotolewa na baraza hilo, Iran imesema Marekani imekubali mpango wa vipengele 10 uliowasilishwa na Tehran, ambao unajumuisha kusitisha mashambulizi ya kijeshi, kuondoa vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa dhidi ya Iran, kulipa fidia pamoja na kuruhusu Iran kuwa na udhibiti wa Mlango wa Hormuz.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ushindi huo umeelezwa kuwa umetokana na uongozi thabiti wa Seyed Mojtaba Khamenei, juhudi za wanajeshi wa Iran pamoja na mshikamano wa wananchi wa taifa hilo katika kipindi cha mvutano wa kijeshi.

Wakati huo huo, mazungumzo rasmi kati ya Iran na Marekani yanatarajiwa kufanyika katika mji wa Islamabad nchini Pakistan kwa muda wa wiki mbili, yakilenga kukamilisha makubaliano ya kusitisha mapigano na kuweka msingi wa amani ya kudumu.

Hata hivyo, SNSC imesisitiza kuwa vita hivyo havijaisha rasmi, na imeonya kuwa mapigano yanaweza kuendelea iwapo masharti yote yaliyowekwa na Iran hayatatekelezwa kikamilifu.

Baraza hilo pia limewataka wananchi wa Iran kuendelea kudumisha umoja na kuwa tayari kwa hatua yoyote itakayochukuliwa endapo mazungumzo hayo hayatatoa matokeo yanayotarajiwa.

Post a Comment

Previous Post Next Post