Urusi Yaondoa Wataalamu Kituo cha Nyuklia Iran Kufuatia Shambulio la Kutatanisha

Urusi imeanza kuwaondoa zaidi ya wataalamu wake kutoka kituo cha nyuklia cha Bushehr nchini Iran kufuatia tukio la shambulio lililoripotiwa kutokea usiku wa Jumanne.

Taarifa hiyo imetolewa na mkuu wa shirika la nishati ya nyuklia la Urusi, aliyesema kuwa hatua hiyo inalenga kulinda usalama wa wafanyakazi wake wanaofanya kazi katika mradi huo.

Kwa mujibu wa Iran, kombora moja lilidondokea ndani ya eneo la kituo hicho, lakini halikusababisha uharibifu wowote. Serikali ya Iran imezituhumu Marekani na Israel kuhusika na shambulio hilo.

Taarifa zinaeleza kuwa watu 163 waliondolewa mapema Jumatano kuelekea mpaka wa Iran na Armenia.

Hadi sasa, takriban wataalamu 300 bado wapo katika eneo hilo, huku wachache wakitarajiwa kubaki kusimamia vifaa muhimu vya kituo hicho.

Kabla ya tukio hilo, Urusi ilikuwa tayari imeondoa wafanyakazi 150 kutokana na hofu ya mashambulizi ya anga kutoka Marekani na Israel.

Urusi ilishiriki kwa kiasi kikubwa katika ujenzi wa kituo cha Bushehr na inaendelea kusaidia uendeshaji wake. 

Wakati huo huo, kazi ya ujenzi wa mitambo miwili mipya ya nyuklia katika kituo hicho ilisimama baada ya mvutano wa kijeshi kuanza.

Hatua hiyo inaashiria kuongezeka kwa taharuki katika eneo hilo, huku mataifa makubwa yakihusishwa moja kwa moja na mgogoro unaoendelea.








Post a Comment

Previous Post Next Post