Mashambulizi Makali Yaibuka Kati Ya Marekani Na Iran Hiki Ndicho Kinacho Endelea Mpaka Sasa

Mvutano kati ya Marekani na Iran umeendelea kushika kasi baada ya Jeshi la Marekani kutekeleza mashambulizi mapya dhidi ya maeneo ya kijeshi nchini Iran, hatua inayozua hofu kubwa ya kuvunjika kwa usitishaji mapigano uliopo kati ya mataifa hayo mawili yenye uhasama wa muda mrefu.........TAZAMA VIDEO HAPA.

Kwa mujibu wa Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani katika Mashariki ya Kati (Centcom), mashambulizi hayo yalilenga eneo la kijeshi lililopo katika mji wa kimkakati wa Bandar Abbas, bandarini muhimu iliyopo kusini mwa Iran karibu na Mlango wa Hormuz. Marekani imedai kuwa eneo hilo lilikuwa likijiandaa kurusha droni nyingine ya mashambulizi wakati operesheni hiyo ilipotekelezwa.

Centcom pia imesema vikosi vyake vilifanikiwa kudungua droni nne za Iran ambazo zilidaiwa kuwa tishio kwa usalama katika eneo la Mlango wa Hormuz, njia muhimu ya usafirishaji wa mafuta duniani. 

Kwa mujibu wa jeshi hilo, hatua hiyo ilikuwa sehemu ya operesheni za kujilinda na kuzuia mashambulizi yanayoweza kuhatarisha wanajeshi wa Marekani pamoja na usalama wa meli zinazopita katika eneo hilo.

Vyombo mbalimbali vya habari vya Iran vilithibitisha kusikika kwa milipuko mashariki mwa Bandar Abbas, huku wananchi wakieleza kushuhudia moshi mkubwa ukifuka baada ya mashambulizi hayo.

Mashambulizi hayo yanajiri katika kipindi ambacho Marekani na Iran ziko katika hali ya usitishaji mapigano wenye sintofahamu kubwa, huku mazungumzo ya kidiplomasia yakiendelea kwa lengo la kumaliza vita vya miezi mitatu vilivyosababisha taharuki kubwa katika Mashariki ya Kati.

Katika kipindi cha miezi hiyo ya vita, shughuli za usafirishaji wa mafuta na biashara kupitia Mlango wa Hormuz zimeathirika kwa kiasi kikubwa. 

Maelfu ya meli za mafuta na biashara zimeripotiwa kukwama katika eneo hilo kutokana na hofu ya mashambulizi, hali iliyosababisha bei za nishati duniani kupanda kwa kasi.

Hii ni mara ya pili ndani ya siku tatu kwa Marekani kushambulia maeneo ya Iran. Mapema wiki hii, Jeshi la Marekani lilitangaza kufanya mashambulizi mengine kusini mwa Iran, yakidaiwa kulenga maeneo ya makombora pamoja na boti zilizokuwa zikijaribu kutega mabomu katika Mlango wa Hormuz.

Post a Comment

Previous Post Next Post