Picha za satelaiti zinaonekana kuonyesha uharibifu katika kambi ya Jeshi la Anga la Israel (IAF) kufuatia mashambulizi ya makombora ya Iran

Picha mpya za satelaiti zilizorekodiwa Jumatatu zimeibua mjadala mkubwa baada ya kuonekana kuonyesha dalili za uharibifu katika Kituo cha Jeshi la Anga la Israel (IAF) cha Ramat David, kilichopo kaskazini mwa Israel, kufuatia mashambulizi ya makombora ya balistiki yaliyorushwa na Iran usiku wa Jumapili.

TAZAMA VIDEO HII

Kwa mujibu wa picha zilizopigwa na satelaiti ya Sentinel-2 ya Tume ya Ulaya na kuchakatwa kupitia mfumo wa Copernicus Browser, eneo moja ndani ya kituo hicho lilionekana kuwa na mabadiliko ya rangi karibu na jengo la kuhifadhia ndege (hangar). 

Wachambuzi wa picha za satelaiti wanasema hali hiyo inaweza kuashiria kuwa jengo hilo lilipigwa au kuathiriwa wakati wa mashambulizi hayo, ingawa ukubwa wa uharibifu bado haujathibitishwa rasmi.

Iran ilirusha jumla ya makombora 24 ya balistiki kuelekea Israel usiku wa Jumapili na asubuhi ya Jumatatu, huku mengi yakilenga maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo. 

Wakati huo huo, waasi wa Kihouthi wanaoungwa mkono na Iran nchini Yemen nao walirusha makombora mawili ya balistiki kuelekea Israel.

Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) lilitangaza kuwa makombora yote yaliyorushwa usiku wa Jumapili yalidunguliwa au yaliangukia maeneo yasiyo na watu. 

Aidha, sehemu kubwa ya makombora yaliyorushwa Jumatatu pia yalizuiwa kabla ya kufikia malengo yake. Hakuna taarifa ya majeruhi iliyotolewa kufuatia mashambulizi hayo.

Post a Comment

Previous Post Next Post