Top News

Lissu Akiwa Gerezani, Atumiwa Ujumbe Huu Mzito na Kumwagiwa Sifa Hii

Aliyekuwa Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, amemuelezea Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Tundu Lissu, kama mmoja wa watu wenye uwezo mkubwa wa kufikiri na kuchangia suluhisho za changamoto za kitaifa, akisisitiza umuhimu wa kuthamini watu wenye maarifa ndani ya jamii.

Alitoa kauli hiyo akiwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika Viwanja vya Mwembetogwa mjini Iringa, ambapo alieleza kuwa historia ya mataifa mbalimbali inaonyesha mafanikio yanapatikana pale viongozi wanapowapa nafasi watu wenye uwezo wa kiakili na ubunifu. 

Msigwa alisema, "Tundu Lissu ni moja ya akili bora katika nchi hii," akisisitiza kuwa viongozi na jamii wanapaswa kutumia rasilimali watu wenye maarifa kwa manufaa ya maendeleo ya taifa. 

Katika maelezo yake, alitumia mfano wa kibiblia kuhusu Yusuf wa Misri, akieleza jinsi alivyoibuka na kutoa majibu ya hekima akiwa gerezani yaliyosaidia taifa la Misri kukabiliana na kipindi cha njaa na changamoto za kiuchumi.

Amesema simulizi hiyo inaonyesha kuwa jamii hupata suluhisho pale inapowathamini watu wenye akili hata kama hawako katika nafasi za juu za uongozi. 

Aidha, Msigwa alidai kuwa baadhi ya viongozi huwa na hofu kwa watu wenye uwezo mkubwa wa kufikiri, hali inayosababisha kuonekana kama tishio badala ya rasilimali ya maendeleo

"Ukiona kiongozi anakimbia watu wenye akili huyo hafai kuwa kiongozi," alisema, akihitimisha ujumbe wake mbele ya wananchi waliopokea kwa shangwe kauli hizo.

Post a Comment

Previous Post Next Post