Macron atoa kauli hii kuhusu nyuklia ya Iran


Hifadhi ya Uranium ya Iran lazima idhibitiwe na kuwekwa chini ya usimamizi thabiti wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA), kufuatia makubaliano mapya kati ya Marekani na Tehran....TAZAMA VIDEO HAPA.

Tamko hili zito limetolewa na Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, akisisitiza kuwa hatua hiyo ndiyo njia pekee ya kuhakikisha usalama wa kikanda na kuzuia uundaji wa silaha za nyuklia.

Kauli ya Macron imekuja saa chache baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kutangaza rasmi kufikiwa kwa makubaliano ya kihistoria yaliyolenga kusitisha mzozo wa kivita katika ukanda wa Mashariki ya Kati.

Macron amebainisha wazi kuwa akiba yote ya uranium iliyorutubishwa iliyobaki nchini Iran inapaswa "kuondolewa kabisa nchini humo au kupunguzwa nguvu yake" (diluted) ili isiweze kutumika kijeshi.

Ufaransa, ikishirikiana na washirika wake wa Ulaya ikiwemo Uingereza, imetangaza kuwa iko tayari kuchukua hatua za haraka ikiwa ni pamoja na kutuma ujumbe wa kijeshi kulinda usalama wa Mlango-bahari wa Hormuz ili kuhakikisha njia hiyo kuu ya biashara ya mafuta inafunguliwa bila vikwazo vya kisheria.

Hatua hii inalenga kuleta utulivu wa kiuchumi duniani huku ikishikilia msimamo thabiti kwamba unafuu wowote wa vikwazo dhidi ya Iran lazima uende sanjari na hatua zinazothibitishwa na wakaguzi wa Umoja wa Mataifa.

Mvutano huu wa kinyuklia umefikia kiwango cha juu baada ya ripoti za hivi karibuni za IAEA kuonesha kuwa Iran ilikuwa taifa pekee lisilo na silaha za nyuklia lililorutubisha uranium hadi kufikia usafi wa asilimia 60.

Kiwango hicho kinatajwa na wataalamu wa kimataifa kuwa kinakaribia kile kinachohitajika kutengeneza bomu la atomiki, jambo ambalo lilizua hofu kubwa ya kiusalama kote duniani. 

Ingawa Tehran imekuwa ikisisitiza mara kwa mara kuwa mpango wake wa nyuklia ni wa malengo ya kiraia, nishati, na matibabu pekee, mataifa ya Magharibi yamekuwa na mashaka makubwa kutokana na kiwango kikubwa cha akiba hiyo ambacho hakina uhalali wa kiuchumi kwa matumizi ya kawaida ya kijamii.

Katika diplomasia hii mpya, kuna ripoti zinazoashiria uwezekano wa Iran kukubali kuhamishia akiba yake ya uranium iliyoboreshwa kwenda nchini Urusi kama sehemu ya makubaliano ya kupunguza vikwazo vya kiuchumi vinavyoikabili.

Tamko la Macron linaweka wazi kuwa Jumuiya ya Kimataifa haitafanya mzaha na usimamizi wa vifaa hivyo hatari, na kwamba macho yote sasa yanaelekezwa Evian, Ufaransa, ambapo viongozi wa mataifa tajiri zaidi duniani (G7) wanakutana kujadili mustakabali wa usalama wa dunia na utekelezaji wa makubaliano haya mapya.

Post a Comment

Previous Post Next Post