FBI Yamnasa Anayetuhumiwa Kutuma Fedha Kwa Kundi La Kigaidi La ISIS

Mwanamume mmoja mwenye umri wa miaka 34, mkazi wa jimbo la Georgia nchini Marekani, amefunguliwa mashtaka ya utakatishaji fedha na kuharibu ushahidi, akituhumiwa kutuma zaidi ya dola 26,000 kwa watu na makundi yanayohusishwa na kundi la kigaidi la Islamic State (ISIS).

Mwanaume huyo aliyetambuliwa kwa jina la Younes Moustafa Younes, anadaiwa kutumia miamala ya fedha za kidijitali (Cryptocurrency) kufanikisha uhamishaji wa fedha hizo kwa watu wanaohusishwa na ISIS, ambao wanadaiwa kuendesha shughuli zao nchini Syria.

Kwa mujibu wa nyaraka za uchunguzi, kati ya Desemba 2025 na Juni 2026, Younes alituma jumla ya dola 16,807 kupitia miamala ya Cryptocurrency kwa lengo la kusaidia shughuli za kundi hilo. 

Inadaiwa alitumia namba mbalimbali za simu na akaunti tofauti ili kuficha utambulisho wake wakati wa kutuma fedha hizo.

Maafisa wa Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) wanasema mtuhumiwa huyo pia alijaribu kuharibu ushahidi kabla ya kukamatwa kwake Novemba 18, 2026.

Wakati wa upekuzi katika makazi yake, gari, vifaa vya kielektroniki na sehemu yake ya kazi, maafisa wa FBI waligundua simu tatu zilizokuwa zimezama ndani ya kimiminika kisichojulikana. 

Simu moja ilikuwa imevunjwa, nyingine namba yake ya utambulisho ilikuwa imeondolewa, huku nyaraka zilizochanwa zikiwa zimezamishwa ndani ya maji yaliyokuwa kwenye beseni la kuogea.

Uchunguzi wa awali unaonesha kuwa FBI ilianza kumfuatilia Younes mwaka 2020 baada ya kubaini kuwa alikuwa akipata na kutazama maudhui ya propaganda za ISIS kupitia mtandao. Alipofanyiwa mahojiano wakati huo, alikiri kutazama maudhui hayo lakini akakanusha kuunga mkono misimamo ya makundi yenye itikadi kali.

Hata hivyo, kwa mujibu wa wachunguzi, baadaye alidaiwa kuanza kuonesha uungwaji mkono mkubwa kwa ISIS na makundi mengine ya kigaidi kupitia mawasiliano yaliyosimbwa kwa njia fiche. Pia alidaiwa kuwa na mawasiliano na watu waliowahi kutiwa hatiani kwa makosa yanayohusiana na ugaidi.

Nyaraka za mashtaka zinaeleza kuwa kati ya Desemba 2021 na Aprili 2022, Younes alifanya miamala 11 yenye thamani ya dola 9,206 kwenda kwenye akaunti za Cryptocurrency kwa kutumia jina bandia. Fedha hizo zinadaiwa kuwa zililenga kusaidia ISIS.

Septemba 2022, mtuhumiwa huyo anadaiwa kuuza gari lake, kuchukua fedha zake za mafao ya kustaafu na kuacha kazi kabla ya kusafiri kwenda Uturuki kwa tiketi ya kwenda tu. 

Inadaiwa aliishi nchini humo kwa takribani miaka miwili kabla ya mamlaka za Uturuki kushirikiana na Marekani kumrejesha nchini humo baada ya kutolewa kwa hati ya kukamatwa kwake.

Endapo atapatikana na hatia katika mashtaka yote mawili, Younes anakabiliwa na kifungo cha hadi miaka 40 jela pamoja na faini inayoweza kufikia dola 750,000.

Kesi yake inatarajiwa kuanza kusikilizwa katika hatua za awali Novemba 23, 2026, mjini Macon, Georgia.

Uchunguzi huo unaongozwa na FBI Atlanta kwa kushirikiana na FBI Newark pamoja na Kituo cha Taifa cha Kupambana na Ugaidi cha Marekani. 

Serikali ya Marekani imeendelea kueleza kuwa inafuatilia vitisho vinavyotokana na watu wanaodaiwa kushawishika na propaganda za makundi ya kigaidi kupitia mitandao ya kijamii na majukwaa ya mawasiliano ya kidijitali.

Post a Comment

Previous Post Next Post