Iraq Yafikia Makubaliano na Wanamgambo Wanaoungwa Mkono na Iran Kudhibiti Mji wa Jurf al-Sakhar, Huku Serikali Ikijaribu Kurejesha Mamlaka Yake

Serikali ya Iraq imeanza kurejesha udhibiti wa mji wa Jurf al-Sakhar, uliokuwa chini ya kundi la wanamgambo la Kataib Hezbollah linaloungwa mkono na Iran kwa takribani miaka 12.

Hatua hiyo imefuatia makubaliano yaliyofikiwa kati ya serikali ya Iraq na kundi hilo siku ya Alhamisi, Novemba 19, 2026, ambayo yalisaidia kuzuia uwezekano wa mapigano kati ya pande hizo mbili.

Mji wa Jurf al-Sakhar unapatikana takribani kilomita 60 kusini-magharibi mwa mji mkuu wa Baghdad, katika jimbo la Babil.

Kundi la Kataib Hezbollah liliteka eneo hilo kutoka kwa wapiganaji wa Islamic State (ISIS) mwaka 2014 na baadaye kulibadilisha jina na kuliita Jurf al-Nasr, linalomaanisha ushindi.

Tangu wakati huo, kundi hilo limekuwa likizuia mamlaka za serikali kurejesha udhibiti kamili wa eneo hilo. Pia, kumekuwa na madai kwamba baadhi ya watu wamekuwa wakitumia eneo hilo kuiba na kusafirisha mafuta kutoka kwenye mabomba ya ndani.

Serikali ilianza kuchukua hatua baada ya ripoti ya kiintelijensia kuhusu biashara haramu ya mafuta katika eneo hilo kutolewa wiki iliyopita.

Waziri Mkuu Ali al-Zaidi aliunda kamati maalumu kuchunguza madai hayo na baadaye kulitaka kundi la Kataib Hezbollah kuondoka katika mji huo kabla ya Ijumaa.

Hata hivyo, siku moja kabla ya muda huo kufika, pande hizo zilifikia makubaliano yaliyowezesha vikosi vya serikali kuingia katika eneo hilo bila kutumia nguvu za kijeshi.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, kituo cha pamoja cha operesheni za usalama kitaanzishwa, huku wanamgambo wa Kataib Hezbollah wakitarajiwa kuondoka hatua kwa hatua.

Vikosi vitakavyotumwa katika eneo hilo vinajumuisha kikosi cha jeshi la Iraq, polisi wa shirikisho, polisi wa usalama wa nishati na vikosi viwili vya Popular Mobilisation Forces (PMF).

Ripoti zinaeleza kuwa Iran ilihusika katika kufanikisha makubaliano hayo kupitia Esmail Qaani, mkuu wa kikosi maalumu cha Quds Force kinachohusishwa na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran.

Serikali ya al-Zaidi imekuwa ikijaribu kurejesha mamlaka ya serikali kuu katika maeneo mbalimbali ya Iraq na kupambana na ufisadi unaodaiwa kufadhili baadhi ya makundi yenye silaha.

Mwezi Mei 2026, al-Zaidi aliingia madarakani akiahidi kupambana na ufisadi na kuhakikisha usalama wa nchi unasimamiwa na serikali.

Awali, aliweka Septemba 30 kuwa mwisho wa muda kwa makundi ya wanamgambo kukabidhi silaha zao chini ya udhibiti wa serikali. Hata hivyo, makundi hayo yalipokataa, muda huo uliongezwa hadi Juni 2027.

Baghdad pia ina wasiwasi kuhusu makundi yenye silaha kutumia ardhi ya Iraq kufanya mashambulizi dhidi ya mataifa jirani kwa maslahi ya Iran.

Tangu kuanza kwa vita kati ya Marekani, Israel na Iran, baadhi ya makundi ya wanamgambo nchini Iraq yameahidi kuunga mkono Iran.

Mtaalamu wa masuala ya Iraq Akeel Abbas alisema hatua ya serikali kuingia Jurf al-Sakhar inahusiana zaidi na usalama wa taifa kuliko biashara haramu ya mafuta.

Alisema eneo hilo limekuwa muhimu kwa shughuli za kijeshi za makundi yanayoiunga mkono Iran.

Hata hivyo, wachambuzi wanaonya kuwa makubaliano hayo huenda yasitoshe kumaliza ushawishi wa wanamgambo.

Mtaalamu wa usalama Tallha Abdulrazaq alisema baadhi ya watu waliotumwa na serikali katika vikosi vya usalama wana uhusiano na makundi hayo, akieleza kuwa mabadiliko hayo yanaweza kuwa ni kubadilisha wanamgambo waliovaa kiraia na kuweka wengine waliovaa sare za serikali.

Kwa upande mwingine, Zeidon Alkinani alisema makubaliano hayo ni hatua nzuri kwa sababu yalifikiwa kupitia mazungumzo badala ya mapigano.

Hata hivyo, alionya kuwa mafanikio yake yatategemea muda unaotumika kurejesha mamlaka ya serikali na masharti ambayo makundi ya wanamgambo yanaweza kudai.

Kwa sasa, serikali ya Iraq inakabiliwa na changamoto ya kuhakikisha kuwa udhibiti wa Jurf al-Sakhar unakuwa wa kweli na si mabadiliko ya majina ya vikosi vinavyosimamia eneo hilo.

Post a Comment

Previous Post Next Post