Marekani Yafanya Mashambulizi Mapya Iran Huku Hofu ya Vita Ikiongezeka

Jeshi la Marekani limefanya mashambulizi mapya dhidi ya Iran kwa kulenga eneo la kijeshi katika mji wa bandari wa kimkakati wa Bandar Abbas, hatua ambayo imeongeza hofu ya kuvunjika kwa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya mataifa hayo mawili yenye uhasama wa muda mrefu.

Kwa mujibu wa United States Central Command (CENTCOM), vikosi vya Marekani pia vilifanikiwa kuangusha drones nne za mashambulizi za Iran ambazo zilitajwa kuwa “tishio” katika eneo la Strait of Hormuz, njia muhimu ya usafirishaji wa mafuta duniani.

CENTCOM ilieleza kuwa eneo lililolengwa Bandar Abbas lilikuwa likijiandaa kuzindua drone ya tano ya mashambulizi wakati operesheni hiyo ilipofanyika. 

Vyombo vya habari vya Iran viliripoti kusikika kwa milipuko mashariki mwa mji huo huku baadhi ya wakazi wakidai kuona moshi mkubwa ukifuka angani baada ya mashambulizi hayo.

Mashambulizi hayo yanakuja wakati Marekani na Iran zikiwa katika hali ya kusitisha mapigano yenye sintofahamu huku mazungumzo yakiendelea kwa lengo la kumaliza vita vya miezi mitatu vilivyosababisha usumbufu mkubwa katika usafirishaji kupitia Mlango wa Hormuz pamoja na kupanda kwa bei za nishati duniani.

Hii ni mara ya pili ndani ya siku tatu kwa Marekani kushambulia maeneo ndani ya Iran huku ikisisitiza kuwa mashambulizi hayo yalifanyika kwa ajili ya kujilinda. 

Mapema wiki hii, jeshi la Marekani lilithibitisha kufanya mashambulizi mengine kusini mwa Iran yakidai kulenga maeneo ya makombora pamoja na boti zilizokuwa zikijaribu kuweka mabomu ya majini katika Mlango wa Hormuz.

Kutokana na mgogoro huo, maelfu ya meli za biashara na mafuta zimeripotiwa kukwama katika eneo hilo kutokana na hofu ya mashambulizi. 

Wachambuzi wa uchumi wanaonya kuwa hali hiyo inaweza kuendelea kuathiri biashara ya kimataifa pamoja na kuongeza bei ya mafuta katika masoko ya dunia.

CENTCOM imesisitiza kuwa mashambulizi hayo yalikuwa “ya tahadhari, ya kujihami pekee, na yenye lengo la kudumisha usitishaji wa mapigano.” Jeshi hilo limesema hatua hizo zililenga kulinda wanajeshi wa Marekani dhidi ya vitisho kutoka kwa vikosi vya Iran.

Hata hivyo, Iran imeyalaani mashambulizi hayo na kuyataja kama “ukiukaji mkubwa wa makubaliano ya kusitisha mapigano.” 

Serikali ya Tehran imeonya kuwa haitaliacha “tendo lolote la uadui bila majibu,” kauli ambayo imeongeza hofu ya kuibuka kwa mapigano makubwa zaidi katika Mashariki ya Kati.

Wakati huo huo, Rais wa Marekani, Donald Trump, ametishia kufanya mashambulizi makubwa zaidi ya mabomu iwapo Iran haitakubali masharti ya Washington katika mazungumzo yanayoendelea.

Wachambuzi wa siasa za kimataifa wanaonya kuwa kuendelea kwa mashambulizi na vitisho kati ya Marekani na Iran kunaweza kusababisha mgogoro mkubwa wa kijeshi utakaoathiri uchumi wa dunia, usalama wa kimataifa pamoja na usafirishaji wa mafuta kupitia Ghuba ya Uajemi.

Post a Comment

Previous Post Next Post