Mashambulizi Makali Yaibuka Kati Ya Marekani Na Iran Hiki Ndicho Kinacho Endelea Mpaka Sasa

Mvutano kati ya Marekani na Iran umeendelea kuongezeka baada ya jeshi la Marekani kutekeleza mashambulizi mapya dhidi ya maeneo ya kijeshi nchini Iran, hatua inayozua hofu kubwa kuhusu kuvunjika kwa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya mahasimu hao wa muda mrefu.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka United States Central Command (CENTCOM), mashambulizi hayo yalilenga eneo la kijeshi katika mji wa kimkakati wa Bandar Abbas, bandari muhimu iliyopo kusini mwa Iran karibu na Strait of Hormuz. 

Marekani ilidai kuwa eneo hilo lilikuwa likijiandaa kuzindua drone nyingine ya mashambulizi kabla ya operesheni hiyo kufanyika.

CENTCOM pia ilisema vikosi vyake vilifanikiwa kuangusha drones nne za Iran zilizotajwa kuwa tishio la usalama katika Mlango wa Hormuz, njia muhimu ya usafirishaji wa mafuta duniani. 

Kwa mujibu wa jeshi hilo, hatua hiyo ilikuwa sehemu ya operesheni ya kujihami iliyolenga kuzuia mashambulizi ambayo yangehatarisha wanajeshi wa Marekani pamoja na usalama wa meli zinazopita katika eneo hilo.

Vyombo mbalimbali vya habari vya Iran vilithibitisha kusikika kwa milipuko mashariki mwa Bandar Abbas huku wakazi wakieleza kuona moshi mzito ukifuka baada ya mashambulizi hayo. 

Hata hivyo, kiwango kamili cha uharibifu pamoja na idadi ya waliopoteza maisha haijathibitishwa rasmi.

Mashambulizi hayo yanakuja wakati Marekani na Iran zikiwa katika hali ya kusitisha mapigano yenye hali ya sintofahamu huku mazungumzo ya kidiplomasia yakiendelea kwa lengo la kumaliza vita vya miezi mitatu vilivyosababisha mvutano mkubwa katika Mashariki ya Kati.

Katika kipindi cha miezi hiyo ya mapigano, shughuli za mafuta na biashara kupitia Mlango wa Hormuz zimeathirika vibaya. 

Ripoti zinaeleza kuwa maelfu ya meli za mafuta na biashara zimekwama kutokana na hofu ya mashambulizi, hali iliyosababisha bei za nishati duniani kupanda kwa kasi.

Hii ni mara ya pili ndani ya siku tatu kwa Marekani kushambulia malengo ya Iran. Mapema wiki hii, jeshi la Marekani lilitangaza mashambulizi mengine kusini mwa Iran yakidai kulenga maeneo ya makombora pamoja na boti zilizokuwa zikijaribu kuweka mabomu ya majini katika Mlango wa Hormuz.

CENTCOM imeendelea kusisitiza kuwa mashambulizi yote yaliyofanyika yalikuwa ya tahadhari na kujihami kwa lengo la kulinda wanajeshi wa Marekani dhidi ya kile ilichokiita vitisho kutoka kwa vikosi vya Iran.

Hata hivyo, Iran imeonyesha hasira kubwa kufuatia mashambulizi hayo na kuishutumu Marekani kwa kuvunja makubaliano ya kusitisha mapigano. 

Serikali ya Tehran imeonya kuwa haitaliacha suala hilo bila majibu na kwamba hatua za Marekani zinaweza kusababisha mgogoro mkubwa zaidi katika eneo hilo pamoja na kuharibu juhudi zote za kidiplomasia zinazoendelea.

Wakati huo huo, Rais wa Marekani, Donald Trump, ameongeza presha dhidi ya Iran baada ya kutishia kufanya mashambulizi makubwa zaidi iwapo Tehran haitakubali masharti ya Washington katika mazungumzo yanayoendelea.

Kauli hiyo imeongeza wasiwasi katika jumuiya ya kimataifa huku wachambuzi wa siasa za kimataifa wakionya kuwa kuendelea kwa mashambulizi na vitisho kunaweza kusababisha vita kubwa zaidi Mashariki ya Kati na kuathiri uchumi wa dunia, hasa sekta ya mafuta na biashara ya kimataifa.


TAZAMA VIDEO.

Post a Comment

Previous Post Next Post