Tajiri namba moja barani Afrika, Aliko Dangote, amesema kuwa mpango wa kujenga kiwanda kikubwa cha kusafisha mafuta ghafi chenye uwezo wa kusafisha mapipa 700,000 kwa siku sasa utaelekezwa nchini Kenya badala ya Tanzania.
Hatua hiyo imezua mjadala mkubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki, huku wengi wakihoji sababu zilizofanya Kenya ichaguliwe kwa mradi huo mkubwa wenye thamani inayokadiriwa kufikia kati ya Dola za Marekani bilioni 15 hadi 17.
Iwapo mradi huo utatekelezwa kama ulivyopangwa, utakuwa miongoni mwa miradi mikubwa zaidi ya uwekezaji katika sekta ya nishati barani Afrika. Kiwanda hicho kinatarajiwa kuzalisha mafuta yaliyosafishwa yatakayokidhi mahitaji ya ndani ya Kenya na pia kusambazwa katika nchi jirani za Afrika Mashariki, jambo litakalosaidia kupunguza utegemezi wa mafuta kutoka masoko ya mbali na kuongeza usalama wa upatikanaji wa nishati katika eneo hilo.
Uamuzi wa kuelekeza mradi huo nchini Kenya umeibua maswali mengi, hasa kutokana na ukweli kwamba Tanzania pia imekuwa ikitajwa kuwa miongoni mwa nchi zenye mazingira mazuri ya uwekezaji katika sekta ya mafuta na gesi. Wadau mbalimbali sasa wanahoji ni mambo gani yaliyoifanya Kenya kuvutia zaidi kuliko Tanzania katika ushindani wa kupata uwekezaji huo mkubwa.
Post a Comment