Mwanaharakati na mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Alphonce Patrick Muyinga, maarufu kama Alphanga Black, amesema kuwa kuitwa mbele ya Kamati ya Maadili ya chama hakupaswi kutafsiriwa kama adhabu au hukumu, bali ni sehemu ya taratibu za kawaida zinazotumika kuhakikisha wanachama wote wanazingatia kanuni na maadili ya CCM.
Akizungumza kuhusu mijadala iliyoibuka kwenye mitandao ya kijamii kufuatia taarifa zinazohusu Kamati ya Maadili ya CCM, Muyinga alisema hakuna mwanachama aliye juu ya chama, hivyo kila mmoja ana wajibu wa kuwajibika pale inapohitajika bila kujali cheo au nafasi aliyonayo ndani ya chama.
Alieleza kuwa Kamati ya Maadili ina jukumu la kusikiliza, kuchunguza na kutoa nafasi kwa wanachama kueleza upande wao kabla ya hatua yoyote kuchukuliwa. Kwa mujibu wake, kuitwa mbele ya kamati si uthibitisho wa kosa, bali ni sehemu ya mchakato wa ndani wa kuhakikisha haki na uwazi vinafuatwa.
Muyinga alisema historia ya CCM inaonyesha kuwa viongozi na wanachama mbalimbali wamewahi kuitwa mbele ya kamati hiyo kwa nyakati tofauti, jambo linalodhihirisha kuwa utaratibu huo ni wa kawaida na si wa kulenga mtu mmoja mmoja.
Post a Comment