Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Jacob Mkunda, amezua mjadala miongoni mwa wananchi na wadau mbalimbali baada ya kutoa kauli inayowahusu maafisa wa jeshi wanaostaafu na ushiriki wao katika masuala ya siasa.
Jenerali Mkunda alitoa kauli hiyo wakati wa hafla ya kuwaaga majenerali waliostaafu kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ambapo alieleza kuwa utaratibu wa kuwaaga wanajeshi wanaomaliza utumishi wao ni sehemu ya utamaduni wa jeshi unaowahusu wanajeshi wa ngazi zote, kuanzia askari wa kawaida hadi maafisa wakuu.
Alifafanua kuwa tofauti iliyopo ni namna ya kuandaliwa kwa hafla hizo kulingana na vyeo vya wahusika, huku akibainisha kuwa baadhi ya majenerali waliokuwa wanaagwa wameitumikia nchi kwa zaidi ya miaka 40, jambo linalostahili kuthaminiwa.
Katika maelezo yake, Jenerali Mkunda alisema matarajio ya jeshi ni kuona maafisa hao wanaostaafu wanaendelea kuishi maisha mazuri pamoja na familia zao baada ya kumaliza utumishi wa muda mrefu serikalini.
Alieleza pia kuwa maafisa hao huendelea kuwa chini ya uangalizi na utaratibu maalumu wa jeshi kwa kipindi cha miaka mitatu baada ya kustaafu kabla ya kuendelea na shughuli nyingine za kiraia.
Post a Comment